ADVERTISEMENT
ADVERTISEMENT

SIASA

KIAMA WALIOFUJA MIRADI CCM KIMEFIKA: BULEMBO

By

on

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, Abdallah Bulembo amesema kiama kwa wanachama waliofuja na kujimilikisha mali na miradi ya chama hicho kimefika.

Wakati Bulembo akisema hayo, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saad Kusilawe, amekihakikishia chama hicho kuwa, atafanya kazi kufa na kupona kuhakikisha kata na majimbo yaliyoangukia katika mikono ya upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, yanarudi CCM. Waliyasema hayo juzi wakati Bulembo akihitimisha ziara yake ya siku tatu katika Mkoa wa Dar es Salaam alipokuwa katika Wilaya za Ubungo na Kinondoni na kukutana na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama na jumuiya za chama katika wilaya hizo.

Bulembo alikuwa akiangalia mchakato wa uchaguzi katika ngazi mbalimbali za chama, kuzungumzia mali za chama na kufafanua kuhusu dhana ya kiongozi mmoja kushika nafasi moja ya uongozi. Alisema wapo baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM waliojitajirisha kwa kuanzisha miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa nyumba, kununua magari na mingine kwa fedha za chama wanapaswa kutambua, kuwa walikuwa wanakula mali za moto zisizolika. “Waliohodhi mali za chama na wengine kujiandikia mikataba isiyo na ukomo; miaka 50, au miaka 100, wajiandae… haiwezekani chama chenye mali nyingi, kikageuka kuwa ombaomba. Kama ulikuwa unaishi kwa pesa za CCM, tafuta mbinu nyingine hizo zama zimekwisha Chama hakina nafasi hiyo tena kwako; utafungwa,” alisema.

Bulembo ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Mbunge na Rais John Magufuli alisema, “Dar es Salaam pekee kuna viwanja zaidi ya 427 vya CCM, lakini hakuna mapato yanayokwenda CCM… Bwana, kama unataka uongozi kwa ajili ya kula pesa za miradi ya chama, bora usigombee; utaangamia na kama unaamini maisha yako ni katika miradi ya chama, acha; muda huo umeisha.”

Kuhusu wapinzani kushika dola, Bulembo alisema licha ya wapinzani kujitahidi kutuma mapandikizi ndani ya CCM, katu hawwezi kukianguisha chama hicho wal wao kushika dola.

Tutatengeneza barabara, nao watapita, tutajenga shule watoto wao watasoma, tutajenga hospitali, wote watatibiwa na huduma nyingine zote, tutatumia wote, lakini wapinzani kwenda ikulu, haiwezekani,” alisema na kuongeza kuwa ikulu sio sehemu ya kwenda kufanyia majaribio. “Urais haujaribiwi. Hata wasaliti mnaosubiri uchaguzi ufike mkimbie; mkienda, CCM itabaki kuwa CCM na itashinda,” alisema. Kusilawe alisema wakati akizungumzia ushindi wa CCM katika chaguzi zijazo kuwa kutokana na usaliti uliofanywa na baadhi ya wanachama wa CCM katika uchaguzi Mkuu uliopita, chama hicho hakitakuwa na huruma wala aibu kwa yeyote aliyehusika.

Facebook Comments

You must be logged in to post a comment Login

Close